Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ,amewataka wananchi kudai umeme badala ya kudai vifaa vya kuunganishiwa umeme kama vile nguzo, waya na transfoma.
Waziri Kalemani ametoa maelekezo hayo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ngazi ya mikoa katika Mkoa wa Mbeya kijiji cha Bara Wilaya ya Mbozi.
“Wananchi jukumu lenu ni kudai umeme msijichanganye kuulizia nguzo au kufuatilia nguzo zipo ngapi, idadi ya vifaa haiwahusu. Wajibu wenu ni kulipia fedha za kuunganishiwa umeme na kudai kupatiwa huduma hiyo,” Amesema Waziri Kalemani.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa, Cosmas Nshenye, amesema kuwa shughuli kuu za kiuchumi za Mkoa wa Songwe ni kilimo hivyo wanahitaji umeme kwa ajili ya kusindika mazao ya kilimo ili kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha Nshenye amewahamasisha wananchi kuunganisha umeme katika nyumba pamoja na kutunza miundombinu ya kusambaza umeme ,kushirikiana na wakandarasi kwa kuhakikisha wanatoa maeneo yao bila kudai fidia ili kupitisha miundombinu ya kusambaza umeme.