Vutankuvute kuhusu uamuzi wa Serikali kuzuia kurushwa moja kwa moja kupitia vituo vya runinga vikao vyote vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefikishwa katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam.

Wananchi 10 jana walifungua kesi ya kupinga agizo hilo la Serikali wakiitaka Mahakama kubatilisha agizo hilo na kulitangaza kuwa kinyume cha matakwa ya Katiba.

Wananchi waliofungua kesi hiyo ni Azizi Himbuka, Perfect Mwasililwa, Rose Moshi, Penina Nkiya, Andrew Mandari, Hilda Sigara, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Kiongozi, Profesa Ferdinand Wambari pamoja na Jaji Sakieti  Kihiyo ambaye jana hakuwepo mahakamani, walalamikaji wanasimamiwa na mawakili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Kibatala na Omari Msemo.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape  Nnauye na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.

Kati ya maombi ya walalamikaji ni pamoja na kuitaka Mahakama kutangaza kuwa raia wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wana haki ya kikatiba ya kujua majadiliano yanayoendelea bungeni kwa mujibu wa ibara ya 18(B), (d) na 29 (1), na kwamba Serikali imekiuka haki ya kikatiba kuzuia bila kuwa na sababu za msingi.

Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nnape Nnauye alitangaza kusitishwa kwa matangazo ya Bunge Live akieleza kuwa kumetokana na gharama kubwa za urushwaji wa matangazo. Kadhalika, Serikali ilizuia vyombo vingine vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge.

Bunge lilianzisha idara maalum ya kurusha matangazo hayo moja kwa moja kwa baadhi ya vikao na kuhariri sehemu ya matangazo hayo ambayo yalirushwa baadae saa tatu usiku kupitia TBC1.

Uamuzi huo wa Serikali ulileta mgongano wa kimawazo na Kambi ya Upinzani walipinga na kuondolewa nje kwa kutofuata kanuni na taratibu za Bunge. Baadhi yao walikubwa na adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa vipindi tofauti.

Makonda atumbua jipu lingine Dar
Video: 'Gwajima Tunamtafuta sana' - Kamanda Sirro