Watu 30 wameripotiwa kupoteza maisha nchini Somalia baada ya kundi la Al-Shabaab kufanya shambulizi la mabomu katika kambi ya jeshi, jimbo la Galmudug, Juni 27, 2021.
Meja Mohamed Awale wa Jeshi la Somalia ameviambia vyombo vya habari kuwa magaidi walitumia magari yenye mabomu kufanya mashambulizi kwenye kambi ya jeshi katika Mji wa Wisil ulioko kwenye jimbo hilo. Hatua hiyo ilisababisha mapigano kati ya kundi hilo na Jeshi la Serikali likiungwa mkono na wananchi wenye silaha.
“Walishambulia kambi ya jeshi wakiwa na magari mawili yenye mabomu na kusababisha mapigano makali ambayo yalidumu kwa zaidi ya saa moja,” alisema.
“Magari yenye mabomu yaliharibu magari ya jeshi letu, wakaazi wa eneo hili walikuwa na silaha waliungana na jeshi kwa pamoja tukawafukuza Al Shabaab,” aliongeza Meja Awale.
Alifafanua kuwa kati ya watu hao 30 waliopoteza maisha kwenye mapambano dhidi ya Al Shabaab, 17 ni askari wa jeshi la Serikali na raia 13.
Kundi la Al Shabaab ambalo ni mshirika wa Kundi la Kigaidi la Al Qaeda limekuwa likiendesha mapigano ya kigaidi kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Lengo lake ni kuongoza Serikali na kuanzisha utawala wa sheria ya dini (Sharia).
Wapiganaji wa kundi hilo wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mabomu na kuua raia na wanajeshi, wakilenga maeneo yenye watu wengi kama hotel, miji na kambi za jeshi.