Utetezi wa tozo ya Shilingi 100 ya mafuta ya Petroli na Dizeli uliotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba kwamba zinaweza kutumika katika miradi mingine, umekosolewa vikali na Wananchi ambao wamemtaka aache kukurupuka bali afikirie ni kwa namna gani tozo hiyo itaikandamiza jamii.
Wakiongea kwa nyakati tofauti na Dar24 Media Wananchi hao wamesema hawaelewi iwapo Viongozi wa Serikali wanatambua uhalisia wa Mtanzania kiuchumi, ikiwemo changamoto za huduma za kijamii wanazopitia, kwani uamuzi wao katika baadhi ya mambo haulengi kuwasaidia zaidi ya kuwakandamiza.
Mfanyabiashara wa Genge, Roida Nashon amesema kwa kutambua shida za Wananchi Rais Samia alitoa ruzuku ya mafuta ya shilingi bilioni 100 kila mwezi na zilisaidia kupunguza makali ya maisha huku akimtaka Waziri Mwigulu afike katika Genge lake na kushinda hapo, ili ashuhudie uhalisia wa kipato anachokusanya kwa siku.
Amesema, “mimi nadhani hawa Viongozi wetu wangekuwa wanapelekwa ‘field’ kabla ya kufikia uamuzi wa jambo lolote, mfano kama anataka kupandisha bei ya mafuta kama hivi aje tupande naye basi la umma, aje tuuze naye genge, aje ashinde na wauza machungwa ili aone kwanza adha wanazopitia, aone miundombinu ya barabara ilivyo, halafu aende na Hospitali awaone kina mama wanavyopata tabu na huduma za afya ndio arudi sasa na mapendekezo Serikalini.”
Kwa upande wake Kondakta wa basi la abiria, Arafa Said amesema, “mwaka jana walipandisha bei ya mafuta wakasema hiyo inatokana na vita ya Urusi na Ukraine, nini kilitokea zaidi ya nauli kupanda, sasa leo anasema tuvumilie tozo hivi angekuwa yeye angeweza? hapa ni kama tujiandae tu kisaikolojia bei ya nauli itapanda tena, vitu vitapanda bei na ugumu utakuwepo maana amegusa eneo baya.”
Waziri Mwigulu akiwa Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu Bajeti kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024, aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu ya mapendekezo ya tozo hiyo ya shilingi 100 akisema itatumika katika miradi mingine, endapo bei ya mafuta itapungua katika soko la Dunia.