Julio Ceasar Mora na mkewe Waldramina Maclovia Quinteros, raia wa Ecuador ndio wanandoa wenye umri mkubwa zaidi duniani, wakiwa wamedumu kwenye ndoa yao kwa miaka 79.
Mora ana umri wa miaka 110 na mkewe Quinteros anatarajia kufikisha umri wa miaka 105 Oktoba mwaka huu. Hivyo, wana jumla ya miaka 214 na siku 358.
Kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness World Records’ kimewataja pia kama wana ndoa walio hai wenye umri mkubwa zaidi.
Mora alizaliwa Machi 10, 1910 na mkewe alizaliwa Oktoba 16, 1915. Walikutana walipokwenda kwenye mapumziko ya shule kwakuwa dada yake Quinteros alikuwa ameolewa na binamu yake Mora. Hivyo, walikutana nyumbani kwa ndugu zao hao ambao walikuwa wameoana.
Baada ya miaka saba ya uhusiano wao wa siri, walifunga ndoa Februari 7, 1941.
Hata hivyo, ndoa yao ilikuwa ya siri pia kwakuwa walionekana kama ndugu waliooana; familia yao haikubariki uhusiano huo.
Wameeleza kuwa baada ya miaka kadhaa ya usiri waliamua kuweka wazi na walipata pingamizi kubwa kwa wanafamilia. Lakini kadiri miaka ilivyokuwa inaendelea familia ilizoea na kukubaliana na hali halisi kuwa wale ni wanandoa.
Wakizungumzia siri ya mafanikio ya kudumu kwa uhusiano wao na kula chumvi nyingi, walisema, “umoja wa kifamilia chini ya kanuni za upendo, kuheshimiana, uaminifu, elimu sahihi inayozingatia thamani ya familia ndio siri ya mafanikio ya uhusiano wetu.”
Wawili hao waliokuwa wanafanya kazi ya ualimu, wamebarikiwa kupata watoto watano, wajukuu 11, vitukuu 21. Kijana wao wa kwanza alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58.