Watu watatu wanaotuhumiwa kupanga na kufanikisha kumuibia Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe begi lililojaa pesa, wamekamatwa na kuburuzwa Mahakamani.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa watu hao ambao mmoja wao ni ndugu yake Mugabe aliyetajwa kwa jina la Constantia Mugabe waliiba begi lenye $150,000 lililokuwa ndani ya nyumba ya mwanasiasa huyo mkongwe.
Wengine waliotajwa walikuwa wafanyakazi wa maeneo ya nyumba ya Mugabe ambao ni pamoja na Saymore Nhetekwa na Johanne Mapurisa waliokuwa wafanya usafi.
Akitoa maelezo mahakamani, mwendesha mashtaka wa Serikali amesema Constantia alikuwa na funguo za baadhi ya vyumba vya nyumba hiyo na kwamba ndiye aliyewasaidia wenzake kuingia ndani.
Imeelezwa kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Desemba Mosi na mapema Januari. Wanadaiwa kutumia fedha hizo kununua magari, pikipiki pamoja na wanyama wa kufuga.
“Johanne Mapurisa alinunua Toyota Camry, na nyumba moja kwa $20,000 kwa kutumia fedha hizo,” mwendesha mashtaka Teveraishe Zinyemba aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Chinhoyi.
“Saymore Nhetekwa alinunua pikipiki aina ya Honda na wanyama wa kufuga ikiwa ni pamoja na nguruwe na ng’ombe kwa thamani ambayo haijawekwa wazi,” aliongeza.
Mugabe mwenye umri wa miaka 94 aliiongoza Zimbabwe akiwa Rais kwa kipindi cha miaka 37.
Mwanasiasa huyo alilazimika kujiuzulu mwaka 2017 baada ya jeshi la nchi hiyo kuingilia kati mgogoro wa kisiasa ndani ya chama cha Zanu-PF.