Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kuwachukulia hatua wamiliki na mawakala wa mabasi wanaopandisha nauli kiholela kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Waitara ametoa maagizo hayo leo alipofanya ziara katika kituo cha mabasi cha Magufuli jijini Dar es Salaam kuangalia hali ya usafiri wa kwenda mikoani ambapo ameagiza abiria waliolipishwa nauli ya juu kinyume na utaratibu katika moja ya mabasi aliyoyakagua, kurudishiwa kiasi walichozidisha.
Aidha Waitara amesema suluhisho la abiria kulanguliwa ni kuanzisha mfumo wa tiketi mtandao na kuahidi kuanza mwakani baada ya kukaa na wadau na kukubaliana ambapo pia amewaonya wamiliki wanaoingiza magari mabovu barabarani katika kipindi hiki na kuagiza ukaguzi ufanyike ili kubaini magari yaliyozuiwa na kuwachukulia hatua za kisheria wamiliki wake.