Wakala wa Vipimo – WMA, kituo cha uhakiki Vipimo, umewataka wale wenye mashaka na dira (mita) zao za maji kufika kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu kuhakiki, ili kujiridhisha iwapo kiasi cha maji anachopata kinawiana na ankara ya maji anayolipa.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Wakala wa Vipimo kituo cha uhakiki Vipimo Misugusugu, Charles Mavunde Kibaha mkoani Pwani, wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kuongeza kuwa uhakiki huo utamsaidia mwananchi kupata maji na kulipa ankara kwa usahihi kulingana na huduma anayopata.

Amesema “Wakala wa Vipimo Tanzania na Kituo cha Misugusugu, wamepewa jukumu hilo na Serikali kwa mujibu wa sheria ya Vipimo sura 340 pia kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi mkuu ya CCM ya mwaka 2020. Sheria ya Vipimo inawataka wasambazaji wa dira za maji na mamlaka za maji kabla hawajamfungia mteja dira kuhakikisha imehakikiwa ili apate huduma ya maji kwa usahihi.”

“Nitoe wito kwa wananchi, Mamlaka za maji na vikundi vya watumia maji wenye wasiwasi wowote, wanataka kuuliza lolote dira za maji mnakaribishwa kwenye Kituo chetu Misugusugu ili kituo kwa kushirikiana na Mamlaka za maji kutatua changamoto hiyo inayohusu dira za maji  ili mwananchi atumie dira hiyo kwa usahihi na apate faida katika matumizi ya maji lakini pia Mamlaka za maji ziweze kutoa huduma nzuri kwa Wananchi,” amefafanua Mavunde.

Aidha, Mavunde pia amezitaka Mamlaka za maji na wauzaji wa dira za maji nchini kuzingatia utekelezaji wa sheria ya Vipimo sura 340 kwa kupeleka dira zao kupeleka kuhakikiwa kabla ya kufungwa kwa mtumiaji.

TANAPA yafafanua tukio Askari kujeruhiwa, yatoa onyo
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 2, 2023