Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa siku 30 kwa taasisi ya kuratibu mpango wa Taifa wa Damu Salama kushirikisha wadau wengine wote wakiwemo Chama cha Msalaba Mwekundu kuhakikisha kinatafuta namna ya kuratibu upatikanaji wa damu salama zaidi ya chupa 550,000 zitakazo tosheleza mahitaji ya hospitali na vituo vya afya hapa nchini ili kunusuru vifo vya wagonjwa vinavyosababishwa na upungufu wa damu.
Aidha amewaonya watumishi wanaofanya biashara ya kuuza damu kinyume cha sheria za nchi na kwamba hata sita kuwawajibisha watakao bainika wanaowashurutisha ndugu wa mgonjwa kutoa damu kabla ya kumhudumia mgonjwa hali inayosababisha kuhamasisha vitendo vya rushwa na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.
Ameyasema hayo wakati akiongoza tamasha la uchangiaji damu kutoka makundi ya vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sambamba na utoaji wa Chanjo za UVIKO 19 ambapo vijana hao wamefanya matembezi ya hiyari wakihamasisha jamii umuhimu wa kujikinga na magonjwa hatarishi.
“Mpango wa Taifa wa Damu Salama hutoa damu bila malipo kwa hospitali zote hivyo wagonjwa wote wanatakiwa kupata tiba ya damu bila malipo yoyote aidha wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa serikali kuwafichua wale wote watakao bainika wanaouza damu salama kwenye vituo vya afya ili wawajibishwe kisheria,” Amesema Dkt. Gwajima.
Amesema kuwa maisha ya mwanadamu yanategemea damu salama ambapo kundi kubwa la watoto chini ya miaka mitano wanahitaji damu kwa asilimia 50 ikifatiwa na kundi la mama wajawazito aslimia 30, ajali mbalimbali ikiwemo waendesha pikipiki bodaboda asilimia 15 na asilimia 5 hupelekwa kwa wagonjwa wa saratani na upasuaji mkubwa wa moyo.
Dkt Gwajima amesema kuwa shirika la afya Duniani linapendekeza kuwa ili nchi iweze kukusanya damu ya kutosha inapashwa kukusanya chupa za damu kutoka kwa asilimia moja ya idadi ya watu katika taifa ambapo hapa nchini inatakiwa kukusanya damu chupa kumi kati ya watu 1000,
Kwa sasa Mpango wa Taifa wa Damu umeweka malengo ya kukusanya damu salama chupa 550,000 ambapo vijana wamekuwa mstari wa mbele kujitolea kutoa damu inayokusanywa hapa nchini kwa asilimia 80 ila kutokana na hamasa ndogo ya wananchi zinakusanywa chupa 312,907 sawa na chupa sita kwa watu 1000.