Mwandishi wa habari za michezo nchini Hispania Guillem Balague anaamini uongozi wa FC Barcelona umeshajipanga na harakati za kumpata mrithi wa Luis Enrique.
Balague amesema hadi kufikia hatua Enrique amethibitisha kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, uongozi wa Barca unatambua njia utakazopitia ili kukamilisha mpango wa kuwa na meneja mwenye viwango ambavyo vitaendelea kuwaweka kwenye mstari wa mafanikio.
Hata hivyo mwandishi huyo ametanabaisha kuwa, anahisi huenda mchakato wa kumsaka meneja mpya huko Camp Nou ukamuhusu meneja wa Athletic Bilbao Ernesto Valverde, aliyekua meneja wa PSG Laurent Blanc pamoja na Mauricio Pochettino anae kiongoza kikosi cha Spurs.
Wengine anaoingia kwenye mchakato huo ni meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman, Jorge Sampaoli wa Sevilla CF na Eusebio Sacristan Real Sociedad’.
“Naamini miongoni mwa watu hawa mmoja wao atatajwa kuwa mrithi wa kiti cha Enrique, kwa ajili ya msimu ujao wa ligi ya Hispania,” Amesema Guillem Balague alipozungumza na Sky Sports.
“Lengo la uongozi wa Barca ni kutaka kuwa na muendelezo mzuri wa kupambana katika ligi ya Hispania na michuano ya kimataifa, ninaamini hofu imetanda miongoni mwa mashabiki kwa kuhisi ni nani atakaewafaa kwa msimu ujao, lakini kwangu sina shaka kutokana na orodha niliyokutajia.
“Miongoni mwa mameneja niliokutajia, naimani wameshaanza kufanya mazungumzo na viongozi wa Barcelona. Hususan kwa Ernesto Valverde na Laurent Blanc.
“Natambua mtu kama Pochettino ni meneja ambaye ana mashabiki wengi sana pale Barcelona, na kama itatokea anapewa nafasi ya kuwa mkuu wa benchi la ufundi atapata ushirikiano mkubwa katika kazi zake.”