Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, ya Nishati ya atomiki (IAEA), na Chakula na Kilimo (FAO), yamepeleka mbegu za mazao kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu, kama sehemu ya juhudi za kupata mbegu mpya zinazoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa taarira iliyotolewa miji ya Virginia – Marekani, Roma – Italia na Vienna – Austria imesema mbegu zilizopelekwa ni za Mtama, Arabidopsis ambayo ni jamii ya kabichi na Haradali ambayo hutumika zaidi kwenye majaribio ya kijenetiki.
Hatua hiyo, imefikiwa wakati ambapo mkutano wa COP27 ukiendelea huko Sharm el-Sheikh nchini Misri wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, kujadili changamoto za kimazingira, ikiwemo madhara ya janga la tabianchi kwenye mifumo ya uzalishaji chakula duniani.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi amesema sayansi ya nyuklia kwa mara nyingine tena inaonesha uwezo wake wa kipekee wa kukabili mabadiliko ya tabianchi na kwamba anatumai jaribio hilo litaleta uvumbuzi na uzalishaji mwingi wa chakula.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, QU Dongyu amesema, “mamilioni ya wakulima wadogo duniani wanahitaji mbegu zenye mnepo na za ubora wa hali ya juu ili waweze kukabiliana na changamoto zinazoongezeka za mazingira ya kilimo.
Amesema, “Sayansi bunifu kama vile kuboresha aina ya mbegu anga za juu kunaweza kuleta mazao yaliyoboreshwa na kufungua njia angavu na yenye nuru zaidi kwa uzalishaji bora siku za usoni, lishe bora, mazingira bora na maisha bora.”