Wawakilishi wa wananchi kaunti ya Kihingo nchini Kenya wamegoma kukalia viti vya plastiki katika vikao vyao na kuamua kufanya mikutano wakiwa wamesimama wakilaani kutopewa kipaumbele cha mazingira bora ya kazi.
Madiwani hao wa Kihingo, Kusini-magharibi mwa Kenya wameweka wazi msimamo wao wa kutokalia viti hivyo vilivyowekwa kwenye jumba la wazi ambalo wanapaswa kufanyia vikao vyao kwa muda wakati jengo lao mahsusi la mikutano likiendelea kukarabatiwa.
Wamesema kuwa hatua hiyo ni aibu na uonevu kwao kwani kwa kipindi cha miezi saba tangu walipoapishwa kufanya kazi za uwakilishi wamekuwa wakikalia viti hivyo na jengo hilo.
Antony Rotich ambaye ni diwani, ameviambia vyombo vya habari kuwa Serikali imewakosea na kuwadhalilisha kwa kipindi kirefu kwa kutojali mazingira yao ya kazi.
The Standard imeripoti kuwa Spika wa kikao cha kaunti hiyo, Philip Wanjohi amesema kuwa wajumbe wamekuwa wakipata shida kubwa kufanya kazi zao katika mazingira hayo, hivyo ameitaka serikali kuhakikisha inakamilisha ukarabati na kuweka viti vizuri kwenye jengo wanalopaswa kufanyia kazi kama wawakilishi wa wananchi.