Naibu Waziri wa maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, ameagiza kamati ya usalama mkoa wa Tabora kuwachukulia hatua wanasiasa na watu wanaochochea wafugaji kuingia katika maeneo ambayo yamezuiliwa na na kuwavamia askari wa wanayama pori.
Amesema hali hiyo imesababisha kuuawa kwa askari wawili katika eneo la misitu ya Isawima wakati walipokuwa wakijaribu kuwaondoa wafugaji hao.
Naibu waziri Kanyusu ametoa kauli hiyo jana mkoani Tabora wakati akizungumza na wafanyakazi walio chini ya wizara ya maliasili na utalii na uongozi wa mkoa wa Tabora.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mgogoro wa misitu ya hifadhi wa Isawima umekuwa ukichochewa na kiongozi wa wafugaji ambaye ni mwanasiasa katika eneo hilo wilayani Kaliua, jambo lililopelekea askari kuvamiwa na kuuawa.
Kanyasu amesema ni vema hatua dhidi ya kiongozi huyo zikachukuliwa kwa ajili ya kuwafanya watumishi wa wizara ya maliasili na utalii na wengine ambao wanashughulikia kulinda maeneo ambayo yamehifadhiwa kufanya kazi katika mazingira salama.
Kwa upande wake Katibu Tawala mkoa wa Tabora, Msalika Makungu amesema tatizo hilo limeshaundiwa kamati ya uchunguzi na wanatarajia kutoa majibu ya kilichobainika na hatua za kuwachukulia wahusika.