Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametaka mpango wa kuweka mabango ya anwani za makazi na postikodi katika mkoa huo ufuate taratibu za sheria zilizowekwa badala ya kufanyika kisiasa.
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo Novemba 5, 2019 wakati akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwa watendaji mamlaka za serikali za mitaa Mkoani Singida ambayo yameandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Amesema mpango huo wa kitaifa ni muhimu katika utekelezaji wake kwani unasaidia pindi itapotokea matukio ya dharula kama vile moto na usafirishaji wa wagonjwa katika maeneo yao yatakayojulikana kwa namba tofauti na ilivyo sasa.
”Naomba jambo hili lisifanyike kisiasa ila lifuate sheria na taratibu kwani katika maeneo mengine lilichelewa kutokana na wanasiasa kutaka majina yao yawekwe kwenye vibao vya mitaa na tukumbuke itasaidia kuyafahamu maeneo kwa ufasaha hata pindi kuna dharula mfano majanga ya moto na wagonjwa,” amefafanua Dkt. Nchimbi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa mpango huo utaweka vizuri mipango miji katika maeneo wanayoishi wananchi na utapunguza migogoro ya ardhi na utambuzi wa makazi ya watu na kupata huduma ikiwemo kupata huduma za kijamii kwa haraka na urahisi.
“Nawaomba wataalamu wa mkoa ambao wamepata mafunzo haya kwenda kufanya kazi hiyo kwa bidii na kwa weledi na mtangulize maslahi ya Taifa mbele maana mpango huu utarahisisha upataji wa huduma za kijamii na kuondoa migogoro,” amebainisha Bi. Nchimbi.
Akiongea katika mafunzo hayo Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati Antonio Manyanda amesema mpango huo ni utekelezaji wa sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 ambayo inalenga kuboresha maisha ya watanzania.
Amesema mpango huo ulianza katika jiji la Arusha kwa baadhi ya kata kuwekewa miundombinu ya anwani kama sehemu ya mfano na baada ya hapo uliendelea katika jiji la Dodoma ambapo ushahidi wa miundombinu unaonekana.
Kwa upande wa Tanzania bara tayari Mikoa ya Arusha, Dar es salaam na Dodoma imeshaingizwa katika mfumo wa anuani za makazi na postikodi huku upande wa Tanzania visiwani mkoa uliofaidika na mpango huo ukiwa ni Unguja.