Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Abel Makubi, ametoa wito kwa wanataaluma wote wa afya nchini kujisajili na kuhuisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaalamu ndani ya miezi sita kuanzia sasa.

Profesa Makubi ameyasema hayo leo Septemba 17,2020 wakati akizungumza na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalamu ya Wizara ya Afya pamoja na wasajili wa bodi zilizo chini ya wizara hiyo,

Katika mkutano huo, amewataka wale ambao wamejiendeleza zaidi kitalaamu kuwasilisha mabadiliko ya vyeti vyao vya viwango katika mabaraza ili kuendelea kutambulika kisheria na kitaaluma.

“Kila mwanataaluma aliyemaliza mafunzo yake ni vizuri awe amesajiliwa katika mabaraza yao, agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika, na uzuri hivi sasa kuna tovuti hivyo mnaweza kupata kujisali , kulipia na baadae kutumiwa vyeti vyenu bila kuchelewa. Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita wawe wamesajiliwa”. Amesisitiza Profesa Makubi.

Aidha Prof Makubi amewapa miezi mitatu wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma katika sekta ya afya bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma wakajisajili ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.

Hata hivyo Profesa Makubi, amewaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa hospitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kuzingatia kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo kwenye sekta zote za afya ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma husika.

Sambamba na hilo Waganga wa tiba asili wametakiwa kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala kwani serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano kwa kuwasaidia kufanikisha malengo yao ya utoaji wa tiba asili.

Waziri mkuu Libya atangaza kujiuzulu
Wakazi Kakonko kupewa bure kambi ya Wakandarasi