Wanawake mkoani Shinyanga wamewashutumu wanaume kwa kuwaozesha watoto wao wa kike bila kuwajulisha na kwa kubadilishana na jagi moja la pombe wawapo vilabuni.
Hayo yamebainishwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, yaliyofanyika katika kijiji cha penzi kata ya Mondo kupitia shirika lisilo la kiserikali la World Vision.
Wamesema kulingana na mila na desturi za kisukuma wanawake hawaruhusiwi kuhoji inabidi wakubali watoto wao waolewe japo wanasoma kwani wakikataa wanaambulia kipigo.
Imeelezwa kuwa kuna wakti mwingine mtoto anakuwa anafanya vizuri kwenye masomo yake lakini baba yake anamtaka afanye vibaya kwa kusingizia kuwa hana fedha ya kumsomesha kumbe anakuwa tayari amekula mahali.
Aidha Afisa maendeleo ya jamii mkoani humo, Tedson Ngwale amesema wataendelea kuhakikisha kuwa hakuna ndoa yoyote itakayo fungwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya bila kuwepo na cheti cha kuzaliwa ambacho kitaonesha umri wa anayekwenda kuolewa na akiwa chini ya mika 18 wazazi wa pande zote mbili watashtakiwa.