Kituo cha sheria na haki za binaadamu (LHRC) kimewataka wakazi wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na serikali za mitaa kuunda vikosi vya ulinzi mitaani kwaajili ya kuwalinda wanawake wasifanyiwe ukatili wa kingono.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mendaji wa LHRC, Anna Henga kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wasaidizi wa sheria na waangalizi wa haki za binaadamu kanda ya Magharibi.
Amesema kuwa pamoja kuundwa kwa vikosi hivyo vya ulinzi, lakini pia wanawake wanaofanyiwa vitendo hivyo nao wanapaswa kutoa taarifa katika vyombo vya usalama haraka pale wanapopatwa na tatizo.
“Hapa Kigoma kuna kitu wanaita tereza, yaani wanaume wanajipaka mafuta ya mawese afu wanawaingilia wanawake kingono kwa nguvu, wanapiga,wanawajeruhi, wanawaibia na wakiwashika wanateleza baada ya kujipaka hayo mafupa, Nimefika Kigoma mwenyewe ili niweze kujionea mwenyewe maana awali nilikuwa nasikia tu hizi habari za tereza, lakini nimeamini hili jambo lipo na baadhi ya waathirika waliofanyiwa vitendo hivyo nimeongea nao naamini tukishirikiana hili jambo litaisha,”amesema Henga
Aidha, amesema kuwa kitendo wanachofanyiwa baadhi ya wanawake wa Kigoma Mjini hasa maeneo ya Mwanga na Katubuka cha kuingiliwa kinguvu kingono, kupigwa na kuibiwa mali zao ni kitendo kibaya mno na hakiwezi kuvumiliwa.
Kwa upande wake Ofisa mratibu wa masuala ya ulinzi na usalama kutoka LHRC, Renatha Selemani amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watetezi wa haki za binaadamu baada ya kuona kuna hatari nyingi za kiusalama zinawakabili.