Wanaume walioko kwenye ndoa wanaowalaghai wanawake wengine itakuwa ‘mwisho Chalinze’, kama mpango wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wa kuanzisha kanzidata (database) ya wanandoa utafanikiwa.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa amepanga kusajili wanaume wote wenye ndoa mkoani humo na kuweka majina yao kwenye kanzidata ili kuondoa tabia ya baadhi ya wanaume waliooa kuwarubuni wanawake wengine wakiahidi kuwaoa.

Makonda amesema mpango huo unalenga kukomesha tabia ya baadhi ya wanaume wenye ndoa wanaowatapeli wanawake kwa ahadi ya ndoa lakini huishia kuwavunja moyo. Kadhalika, baadhi ya wanaume wenye ndoa hufunga ndoa nyingine kwa siri.

“Wakina dada wa mkoa wa Dar es Salaam wengi wamechoka kutapeliwa, vijana na wanaume wamekuwa wakiwaahidi kuwaoa halafu wanaingia mitini. Jambo hili linafedhehesha kidogo na wamefanya watoto wengi wamekuwa na majeraha moyoni, yaani wewe kaka unamdanyanganya dada wa watu anategemea unataka kumuoa kumbe unamtapeli tu,” alisema Makonda.

“Kanzidata hii itawasaidia wanawake wasitapeliwe, ukitaka kumuoa mtu anaenda mtandaoni kuangalia taarifa zako. Hapo atabaini kama umeoa au la; na vilevile itasaidia hata wanawake ambao wameolewa ili wanaume wao wasioe kwa siri,” Makonda anakaririwa.

Amesema atatumia mkutano wa SADC ili kupata uzoefu kutoka kwenye nchi nyingine kuona jinsi wanavyoshughulika na tatizo kama hilo ili mpango huo ufanikiwe. Pia, amesema atatumia kifungu cha sheria kinachowalinda wanawake dhidi ya ulaghai wa wanaume.

Makonda ameweka wazi mpango wake wa kukutana na wanawake wa mkoa huo ambao wamevunjwa moyo na wanaume waliowatapeli kwa kutumia mtindo huo.

Hivi karibuni, kupitia mitandao ya kijamii, kumekuwa na taarifa za wanaume kufunga ndoa huku wakijitokeza wanawake wengine ambao hudai ni wake zao.

Matukio mengine ni baadhi ya matukio ya kufunga ndoa kuzua mzozo baada ya wanawake wengine kuibuka na kupinga uhalali wa ndoa hizo hata kama wao hawakufunga ndoa rasmi na mhusika.

DC aamuru wachimbaji wa madini kuswekwa ndani
Exclusive: Waziri Mhagama, Askofu Mkude waelezea funzo la ajali ya Morogoro (Video)