Serikali imetoa wito kwa wanaume wanaonyanyaswa na wake zao kijinsia kujitokeza kutoa taarifa hizo kwenye madawati ya kijinsia yaliyo karibu na makazi yao.
Wito huo umetolewa na Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Dk, Faustine Ndungulile, alipo kuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalum CCM, Rita Kabati.
Katika swali lake, Rita alitaka kujua lini Serikali itatunga sheria ya kuwatetea wanaume ambao wapo kwenye jamii na wananyanyaswa kjinsia na wake zao wanaoishi nao.
Dk. Ndungulile amesema kuwa yapo madawati yanayoshughulikia masuala ya unyanyasaji katika vituo vya Polisi na maeneo mbalimbali nchini hivyo tatizo kubwa lipo kwa wanaume kutojitokeza kulalamikia vitendo hivyo na badala yake hukaa kimya.
Aidha ametoa ufafanuzi kuwa Serikali inatambua ukatili wa kijinsia ni pamoja na vitendo vya kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwadhulumu wanawake na watoto.
Ameeleza pia ukatili wa kingono na kisaikolojia ni sehemu ya ukatili wa kijisia, hivyo ni muhimu kutolewa taarifa na moja ya hatua ambayo Serikali imechukua ni pamoja na kuandaa mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/2015- 2021/22.
Mpango ambao unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022 .
Sheria hiyo inatoa fursa kwa wanawake waliofanyiwa unyanyasaji au kudhulumiwa kupata haki zao kupitia vyombo vya sheria bila kujali uwezo wao kuichumi.