Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, Taifa la Misri limeandika historia baada ya kuwaapisha wanawake 98 kuwa majaji.
Majaji hao ambao waliapishwa rasmi Jumamosi, Machi 5, watahudumu katika nyadhifa tofauti kwenye Baraza Kuu la Kisheria nchini humo.
Kuapishwa kwao kulijiri baada yao kuteuliwa mnamo Machi 2021, kufuatia agizo lililotolewa na Abdel Fatah al-Sisi Rais wa Nchi hiyo, katika katika harakati ya kuwawezesha wanawake kufikia nyadhifa tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari nchini humo, majaji hao wa kike wamepewa mafunzo kikamilifu kuhusu taratibu za kisheria, utathmini wa kesi zinazowasilishwa kwao, uendeshaji wa vikao vya kusikiza kesi, masuala ya ufisadi na usalama wa kitaifa.
Kabla ya kula kiapo, majaji hao wa kike walionyesha furaha yao kwa kile walichokitaja kuwa tukio kubwa la kihistoria.
Kuapishwa kwao kumesifiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, maafisa wa serikali na vyama vya wanawake wanaohudumu katika idara ya mahakama.