Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifello Sichwale amesema kuwa wanawake wanaonekana kuwa na hatari kubwa ya kupata matatizo Sugu ya Figo ukilinganisha na wanaume.

Dkt. Sichwale amebainisha hayo Marchi 10, katika maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yaliyofanyika Kitaifa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi, Kibaha.

“Tafiti zinaonesha kuwa kati ya asilimia 11 hadi 17 ya watu wote wanaoishi Afrika hususan kusini mwa jangwa la Sahara wana ugonjwa wa figo, ambapo ugonjwa huu hutokea kwa mwanamke 1 kati ya 4 ukilinganisha na kutokea kwa ugonjwa huu kwa wanaume ambapo takwimu zinaonesha kuwepo kwa mwanamme 1 kati ya 5 wenye umri kati ya 65 mpaka 74 kuishi na ugonjwa wa figo,” amesema Dkt. Sichwale

“Hapa Tanzania kupitia utafiti uliofanyika mwaka 2013 katika jamii ulionyesha kuwa asilimia 7 ya watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo na tafiti zinaonesha kuwa wagonjwa wengi wenye tatizo la figo pia walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.” Dkt. Sichwale ameongeza.

Katika kijikita kuhudumia wagonjwa hao serikali imesema inatarajia kupeleka mashine za kisasa za uchujaji wa damu ‘dialysis’ katika hospitali 12 za Rufaa nchini katika Awamu ya pili ya upanuzi wa Huduma hiyo.

Dkt. Sichwale amesema mpaka sasa jumla ya TZS bilioni 4.9 zitatumika kujenga vituo vinne vipya vya ‘dialysis’ na kukarabati majengo saba yatakayowekewa mashine hizo na hadi sasa mashine za dialysis 110 na mashine za kuchakata maji 11 zimeanza kusimikwa katika hospitali husika.

“Hospitali hizo ni hospitali za mikoa za Songea, Morogoro, Mwananyamala, Temeke, Amana, Tumbi, Mawenzi, Chato, Dodoma, AICC-Arusha na Mbeya,” amebainisha Dkt. Sichwale.

Amesema mipango iliyopo ni kwamba Ifikapo Juni, 2023 hospitali zote za Rufaa nchini zitakuwa zikitoa huduma za usafishaji damu (dialysis) na hivyo kusogeza huduma hii karibu na wananchi hali itakayoongeza kiwango cha watu wanaofanyiwa dialysis kutoka asilimia 32 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo June 2023.

Awali Dkt. Sichwale alidokeza kuwa kabla ya awamu ya kwanza ya upanuzi wa huduma hiyo katika hospitali za rufaa za mikoa, mashine zilipatikana Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hospitali za Kanda na Hospitali Maalum pekee.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha asilimia 10 ya watu wote duniani wanaishi na ugonjwa wa figo ambao ni sugu na tatizo ni kubwa zaidi kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 75 ambapo asilimia 50% ya watu hao wana ugonjwa wa Figo. 

Mauzo ya madini Tanzania yaweka historia, ni 'Matrilioni'
Aliyepandikizwa moyo wa nguruwe afariki dunia