Waratibu wa tuzo ya mpira wa dhahabu (Ballon d’or) France Football magazine, wametangaza kipengele cha mchezaji bora wa kike, ambacho kitakua miongoni mwa vipelenge vitakavyoshindaniwa katika tuzo za mwaka huu 2018.
Uongozi wa France Football magazine umesema kipengele hicho kipya kitajumuisha washiriki 15, na oriodha yake itatangaza sambamba na ile ya wachezaji 30 watakaoingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo ya Ballon d’Or kwa wanaume.
Orodha ya vipengele hivyo viliwi zitatolewa mwezi ujao, na baadae zitachujwa na kufikia idadi ya wachezaji watatu kila upande, kabla ya kutangazwa mshindi katika hafla itakayofanyika Disemba 08 mjini Paris.
Kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 1956, kumekua hakuna kipengele cha mchezaji bora wa kike.
Baada ya kutangazwa kwa hatua hiyo, beki wa klabu ya Olympique Lyonnais kwa wanawake Wendie Renard ameliambia jarida la French Magazine kuwa: “Ni hatua nzuri kwa maendeleo ya soka la wanawake, kwa kipindi kirefu tulihitaji kitu kama hiki, ili kutuongezea ufanisi na kujituma tunapokua uwanjani, kuanzishwa kwa tuzo za wachezaji kwa wanawake naamini itaongeza chachu kubwa.”
Kwa upande wa mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Brazil Marta amesema: “Mara kadhaa nilitamani kuona na wanawake wanaingizwa katika tuzo za Ballon d’Or, naamini wahusika wamesikia kilio cha wanawake na wamefanikisha kilichokua kinakusudiwa.”
Tuzo ya Ballon d’Or ilikua ikitolewa kwa ushirikiano wa FIFA na French Magazine kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, na baada ya hapo kila mmoja amekua akifanya shughuli zake binafsi.