Wanawake nchini wametakiwa kujiwezesha kiuchumi, kijamii na kisiasa ili wapate fursa ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ambayo yatawaletea ukombozi wao na taifa.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA), Edda Sanga alipokuwa akizungumzia mada kuhusu mapambano ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Sanga amesema kuwa unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake kwa sasa umepungua kwasababu chama chake kimefanya juhudi kubwa ya kuwaelimisha wananchi kuhusu kutoa taarifa wanapoona kuna tatizo ili liweze kushughulikiwa mapema iwezekanavyo.

“Chama cha TAMWA kimevitumia vyombo vya habari kutoa hamasa, kuelimisha na kufanya utafiti wa kina kueleza ukatili huu, na hatimaye wahusika kufikishwa katika vyombo vya dola” amesema Sanga.

Aidha, Sanga amebainisha kuwa mkoa wa Mara kuwa ndio mkoa sugu kwa unyanyasaji na ukatili wa wanawake. huku akitolea mfano wa Mama Neema Wandibe ambaye amefanyiwa ukatili wa kupindukia na usiokubalika na mumewe hivi karibuni kwa kummwagia maji ya moto, kwasababu alichuma mahindi mawili shambani na kuyachoma.

Hata hivyo, Sanga amewataka wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana na vyombo husika katika kutoa taarifa na kwamba wanahitaji kujenga jamii yenye malengo kwa ajili ya kuondoa madhara ya unyanyasaji na ukatili wa wanawake.

 

Video: Meya wa Kinondoni azindua mashindano ya mpira Kata ya Msasani
Pombe za viroba zenye thamani ya bilioni 10.8 zakamatwa Dar