Wanawake wanne jijini Beijing nchini China wamenyoa nywele zote na kubaki kipara, katika hatua ya kupinga wanaharakati wanne ambao ni waume zao kufungwa gerezani bila kufikishwa mahakamani.
Wanawake hao ambao mmoja kati yao ni mke wa mwanaharakati maarufu, Wang Quanzhang anayeshikiliwa gerezani tangu mwaka 2015 bila kufikishwa mahakamani, wamedai kuwa wameamua kunyoa nywele zao zote kama ishara ya kupinga matumizi ya mabavu kwani wamezuiwa hata kufungua kesi mahakamani kudai dhamana.
Mke wa mwanaharakati Wang Quanzhang aitwaye Li Wenzu amesema kuwa ameshaenda zaidi ya mara 31 kwenye Mahakama Kuu ya nchi hiyo kujaribu kufungua kesi, lakini polisi wamekuwa wakimzuia kuingia ndani ya eneo la Mahakama hiyo.
Jana, wanawake hao walifika katika eneo la Mahakama hiyo wakinyoa vipara, na baada ya kuzuiwa kuingia ndani walipaza sauti zao wakisema “nchi haiwezi kuendeshwa bila kufuata sheria.”
Wang alikamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama nchini humo kwa madai kuwa ameidharau Serikali, ambapo alikamatwa pamoja na wanasheria wengine watatu waliokuwa wanaharakati wenzake na wakosoaji wa Serikali.