Katika kuadhimisha siku ya Malaria Duniani, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amegawa vyandarua kwa wanawake zaidi ya 400 pamoja na kufikia makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii ndani ya Manispaa ya Shinyanga.
Dkt Molel ameungana na mwenyeji wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini katika Warsha iliyohudhuriwa na wanawake zaidi ya 400.
Katika Warsha hiyo iliyofanyika April 24, 2022 Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imelenga kuboresha huduma za uzazi, mama na mtoto na kuhakikisha jamii inapata elimu ya kutosha na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Asante wakina mama mliokuja hapa kupata elimu ili mkatusaidie kuelimisha wengine na kupunguza vifo vya akina mama na watoto” amepongeza Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Amref kuja na mkakati huo wa kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuweza kutoa misaada mbalimbali inayogusa maisha ya Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel Bi. Doris Mollel amesema kuwa lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu ya ugonjwa malaria na namna ya kujikinga pamoja na kuhamasisha wanawake kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19 ili waweze kujikinga janga hili kubwa la korona, tunaliona linaisha ila bado ugonjwa upo
“Zoezi limefanyika katika mikoa mitatu kwa kushirikiana na Amref kwa mikoa ya Simiyu, Kagera na Shinyanga na tunaishukuru Serikali kwa kutuwekea mazingira wezeshi sisi taasisi binafsi kuweza kufanya kazi na kutoa mchango wetu ndani ya jamii” amesema Doris Mollel.