Wakati Mbeya City ikiendelea kujitetea kutokushuka daraja msimu huu, Uongozi wa Klabu hiyo ya jijini Mbeya wamenza mazungumzo na aliyekuwa Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba aliyeachana na Geita Gold, ili akinoe kikosi hicho.
Taarifa zinaleeza kuwa uongozi wa Mbeya City huenda usimpatie mkataba mpya kocha, Abdallah Mubiru endapo atashindwa kuinusuru timu hiyo na janga la kushuka daraja.
Hata hivyo alipotafutwa Wandiba kuhusu taarifa hizo amesema zipo timu tano ambazo zinahitaji saini yake lakini suala la wapi ataenda msimu ujao litajulikana Juni 30 baada ya mkataba wake uliopo na Geita Gold kuisha.
“Huu ndio wakati wa mambo hayo kuzungumzwa lakini kwangu mimi nina ofa kutoka timu tano hivyo nitaamua pa kwenda endapo nitaona ni sehemu salama kwangu kunitimizia mahitaji yangu,” alisema.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amesema kwa sasa hawawezi kusema lolote juu ya hilo, kwani bado wana michezo ya play-off, hivyo nguvu wamezielekeza huko kwanza.
Wandiba aliondoka Mbeya City Januari 6, mwaka jana na kujiunga na Geita Gold akiwa msaidizi wa kocha mkuu, Fredy Minziro huku akiwahi pia kuzifundisha timu za Singida United na Alliance FC.