Mashetani wekundu (Man utd) wataendelea kumkosa kiungo wao mahiri kutoka nchini Ufaransa Paul Pogba, katika mchezo wao wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya West Bromwich Albion.

Pogba alikosa mchezo wa majuma mawili yaliyopita dhidi ya Middlesbrough baada ya kuumia misuli ya paja katika mpambano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora wa Europa league dhidi ya Rostov.

Meneja Jose Mourinho amethibitisha kuendelea kumkosa kiungo huyo, alipozungumza katika televisheni ya Man Utd, ambapo amesema Pogba anaendelea kupatiwa matibabu na huenda akamtumia kwenye michezo ijayo.

Mourinho amesema mbali na Pogba, pia atawakosa mabeki wa kati Chris Smalling na Phil Jones ambao kwa pamoja walipatwa na majeraha ya miguu baada ya kugongana wakiwa kwenye mazoezi ya timu ya taifa ya England juma lililopita.

Wengine waliotajwa na meneja huyo kutoka nchini Ureno, ni mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic anayetumikia adhabu ya kufungiwa na FA na kiungo Ander Herrera aliye majeruhi.

Man Utd wanakwenda katika mpambano wa jumamosi dhidi ya West Brom wakitambua umuhimu wa kushinda, ili kujipatia point tatu ambazo zitaendelea kuwaweka kwenye mustakabali mzuri wa kuziwania nafasi nne za juu katika msiamamo wa ligi ya England.

Mchezo kati ya Liverpool dhidi ya Everton (Merseyside Derby) unatazamwa kwa macho mawili kama sehemu ya kuisaidia Man Utd kufikia lengo la kuendelea kupanda kwenye msimamo wa ligi, lakini hilo litatokea endapo Liverpool watapoteza dhidi ya wapinzani wao.

Liverpool ipo katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ya England kwa kufikisha point 56 ikifuatiwa na Man Utd yenye point 52.

Mahakama yatengua hukumu ya Mbunge Lijualikali
Vita Yaibuka Chelsea, Ni Alvaro Morata Vs Romelu Lukaku