Wafanyakazi wanne wamekamatwa nchini Kenya kwa tuhuma za kuiba mayai yenye thamani ya $25 kutoka kwenye shamba la Makamu wa Rais wa nchi hiyo, William Ruto.
Uchunguzi umebainisha hayo mara baada ya msimamizi wa shamba hilo lililopo Sugoi mkoa wa bonde la Ufa kutoa taarifa katika jeshi la polisi la nchi hiyo.
”Uchunguzi wetu wa awali umefichua kwamba wafanyakazi wanne wanaoishi ndani ya shamba hilo walihusika katika wizi huo lakini wote wamelikana hilo,”amesema kamanda wa polisi wa eneo hilo, Zachariah Bittok
Aidha, taarifa zinasema kuwa watuhumiwa hao ambao ni wanaume wawili na wanawake wawili wanashikiliwa na polisi katika kituo kimoja kilichopo eneo hilo kwaajili ya mahojiano.
Taarifa hizo zimepokelewa kwa hisia tofauti nchini humo huku baadhi wakikejeli na kusema kwamba kuna mambo ya muhimu zaidi ya kuzungumzia kwenye vyombo vya habari kuliko taarifa za kupotea kwa kreti 10 za mayai ya Ruto.
Hata hivyo, Inaarifiwa kuwa watuhumiwa hao sasa watafikishwa mahakamani, na kreti hizo za Mayai zilizopatikana zitatumika kama ithibati au ushahidi kortini.