Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo oktoba 17, 2021 orodha ya awamu ya kwanza ya wanafunzi waliopangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 99.9 kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru ambapo amesema katika wanafuzi hao, wanaume ni 23,379 sawa na asilimia 62 na wanawake ni 14,352 sawa na asilimia 38.
Badru ameongeza kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopata mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi waliopata mikopo hiyo kupata taarifa kuhusu kiais cha mikopo yao kupitia akaunti walizotumia kupata mikopo hiyo maarufu kama SIPA.
Amesema Serikalia imezitoa fedha hizo mapema ili kuwafanya wanafunzi waende kujiandaa mapema na fedha hizo watazikuta vyuoni ili waanze kutimiza ndoto zao za kielimu.