Waokoaji wanajaribu kuvifikia vijiji vilivyo pembeni zaidi ya nchi ya Msumbiji ambavyo vimeshambuliwa na kimbunga Kenneth chenye nguvu kubwa.
Maelfu ya watu wanahofiwa kuwa wamekwamba katika maeneo yenye nvua kubwa na upepo ambao unaongeza hatari ya kuwepo kwa maporomoko ya ardhi.
Kimbunga Kenneth kilishambulia siku ya Alhamisi kikiwa na kasi ya Kilometa 220 kwa saa (220km/h), ikiwa ni mwezi mmoja tangu kimbunga Idai kishambulie nchi tatu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 900.
Maelfu ya makazi ya watu yameharibiwa, miundombinu ya barabara na umeme pia imeharibiwa vibaya na kusababisha mawasiliano kuwa magumu.
Kwa mujibu wa BBC, zaidi ya watu 20,000 wanaishi katika makazi ya muda kwenye vituo maalum baada ya makazi yao kuharibiwa. Vituo hivyo vimewekwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na shule na makanisa.
Katibu mkuu wa shirika la msaada la kimataifa Amnesty International, Kumi Naidoo amewaambia waandishi wa habari kuwa aina hizo mbili za vimbunga vimetokana na mabadiliko ya tabia nchi, hususan uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli mbalimbali za binadamu kama wanasayansi walivyowahi kuonya.