Waombolezaji jijini Kampala nchini Uganda wameibua tafrani na kuwashambulia vigogo wa Jeshi la Polisi katika msiba wa aliyekuwa Kamanda wa polisi wa mikoa mbalimbali nchini humo, Muhammad Kirumira (pichani) aliyeuawa Jumamosi iliyopita kwa kupigwa risasi.

Afande Kirumira, ambaye aliibuka kuwa mkosoaji mkubwa wa jeshi la polisi akidai kujitoa kufichua uovu unaofanywa na genge la wahalifu waliojificha ndani ya jeshi hilo, alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lake nje ya mji wa Bulenga anakoishi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kuaminika nchini humo, msemaji wa jeshi la polisi, Emilian Kayima alifukuzwa na waombolezaji wenye hasira.

Waombolezaji hao pia walimshambulia Waziri Jeje Odongo ambapo inadaiwa kuwa msemaji wa polisi alijeruhiwa katika matukio hayo. Kadhalika, imeripotiwa kuwa vijana walishambulia magari manne ya polisi yenye mabomu ya machozi yaliyokuwa kwenye viwanja vya eneo la maombolezo.

Ibada ya kumuombea marehemu ilifanyika katika msikiti wa Old Kampala na baadaye mwili ulisafirishwa eneo la mazishi. Waombolezaji walikuwa wakishangilia kwenye mji wa Bulenga wakitumia msemo maarufu unaotumiwa na mbunge Robert ‘Bobi Wine’ Kyagulanyi, “people power – our power.”

Kufuatia tukio la kupigwa risasi kwa kigogo huyo wa zamani aliyejiuzulu nafasi yake na kufunguliwa mashtaka mbalimbali mahakamani, Rais Yoweri Museveni alitoa tamko kali akilaani mauaji hayo na kuahidi kuwa waliohusika watatafutwa kwa nguvu zote na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni

Rais Museveni katika salamu zake za rambirambi, aliahidi kuwa wakati Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha inaweka kamera katika maeneo mbalimbali, itafanya mpango wa kiusalama utakaopambana na wauaji hao aliowaita ‘nguruwe waoga’.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma Septemba 10, 2018
Video: Benki kuu yajibu hoja ya Zitto, Magufuli amgomea Waziri wake