Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Watendaji wa Kata na Wenyeviti wa Vijiji kutoonea wananchi wanaostahili kunufaika na Mpango wa Serikali wa kuziinua Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku akiwataka kutoa taarifa sahihi za watu wanaostahili kupata fedha hizo ili waweze kujikwamua kiuchumi kama lilivyo lengo la Serikali.

Ndejembi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kondo wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani ambao ni wanufaika wa mradi wa TASAF, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wanaokwamisha wananchi wenye sifa kupata fedha hizo kwani wanapokea malalamiko kwa watu kuwa wanaondolewa kwenye orodha.

Aidha amewaonya wale wote waliyo na tabia hiyo huku akisisitiza hatua kali za kisheria zitachukuliwa juu yao kwa wote watakao bainika

Hata hivyo Naibu Waziri Ndejembi amewaagiza Maafisa Kilimo, Uvuvi, Biashara na Maendeleo ya Jamii kuwatembelea wanufaika wa TASAF ili kuwapa mbinu mbalimbali za nini cha kufanya wanapopata fedha hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah amemuahidi Naibu Waziri Ndejembi kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa maagizo yake kwa Maafisa Kilimo, Uvuvi na Biashara ili kuweza kuwasaidia wanufaika wa TASAF kutumia fedha wanazopata kuboresha maisha yao.

Askari aliyesifia gongo afukuzwa kazi
Ujenzi wa daraja jipya la Simiyu wanukia