Chama cha upinzani nchini Nigeria kinachofahamika kama Labor Party, kimedai kuwa tukio la wasichana wa shule wa eneo la Chibok walioripotiwa kutekwa na kundi la kigaidi la Boko Haram lilipangwa kwa malengo ya kisiasa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Abdulkadir Abdulsalami amedai kuwa tukio hilo lilifanywa na wanasiasa kwa lengo la kumchafua Rais aliyekuwa madarakani, Goodluck Jonathan ili ashindwe kwenye uchaguzi mkuu.
Hivyo, kiongozi huyo wa Labor Party aliwataka viongozi wa chama tawala nchini humo kutojisifia kwa kufanikisha kuwarejesha wasichana hao kutoka mikononi mwa Boko Haram kwani lilikuwa tukio la kupangwa.
Alidai kuwa mpango wa chama tawala ni kuhakikisha wanawaachia wasichana hao kwa mafungu hadi itakapofika mwezi Mei mwakani.
“Ikifika Mei 29 mwakani, watawaachia wasichana wote waliobaki. Lakini ukweli utabaki pale kama nilivyowahi kusema wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 kuwa hawa wasichana hawakutekwa na Boko Haram. Waliandaliwa na kutengenezewa tukio kwa lengo la kuchafua taswira ya Goodluck Jonathan,” alisema.
Aprili mwaka 2014, wasichana 276 wa shule za sekondari eneo la Chibok jimbo la Borno waliripotiwa kutekwa na kundi la kigaidi la Boko Haram. Tukio hilo lilitia simanzi sehemu kubwa ya dunia ambapo ilianzishwa kampeni iliyobatizwa jina la ‘Bring Back Our Girls’ kwenye mitandao.
Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana kujaribu kuwaokoa wasichana hao tangu wakati huo, na wamekuwa wakiachiwa kwa mafungu baada ya kundi la Boko Haram kuripotiwa kuishiwa nguvu.