Viongozi wa vyama sita vya upinzani nchini , leo wametoa tamko la pamoja kuhusu hali ya kisiasa nchini na kuweka msimamo wa namna watakavyoendesha shughuli zao mwaka 2019.

Kupitia tamko lao lenye majina ya viongozi wa vyama sita vya siasa ikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), NLD, NCCR Mageuzi, CHAUMMA, ACT Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamedai kuwa mwaka kesho utakuwa mwaka maalum wa kudai uhuru wa kidemokrasia na wameuita ‘Mwaka wa Demokrasia’.

Wameeleza kuwa hawatakubali tena zuio la kufanya mikutano ya hadhara nchini kwa madai kuwa ni haki yao ya kikatiba na kwamba watautangazia umma namna ambavyo watafanya mikutano hiyo kila kona ya nchi.

“Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu, hatutaruhusu katazo haramu na lisilo na mashiko ya kisheria litumike kutuzuia kutekeleza wajibu wetu,” limeeleza tamko hilo.

Serikali ilizuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara isipokuwa kwa wabunge na madiwani waliochaguliwa ambapo wanaruhusiwa kufanya mikutano hiyo katika maeneo waliyochaguliwa.

Aidha, viongozi hao wameeleza kuwa wataunda Kamati Maalum ambayo itafanya shughuli ya kuratibu na kuwafikia wananchi kupitia makundi mbalimbali kwa lengo la kuwaunganisha na kuwapa ari ya kudai haki zao.

Katika hatua nyingine, wametangaza kuwatambua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Mbunge wa Tarime vijijini kama wafungwa wa kisiasa na kwamba watalifuta tangazo lao pale tu watakapoachiwa huru.

Tamko hilo limekuja kufuatia kikao cha siku tatu kilichofanyika kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 18 visiwani Zanzibar.

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 19, 2018
Wanawake wanyoa vipara mbele ya mahakama wakidai waume zao