Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amewapongeza Wabunge wa Zanzibar kwa kutumia vyema nafasi zao za uwakilishi wa majimbo yao ambapo juhudi hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Agosti 24, 2023, wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kilichopokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais katika Ofisi za Bunge Jijini Dodoma.
Amesema, juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi imetokana na mshikamano mkubwa unaofanywa na Wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusemea na kutetea hoja mbalimbali.
“Leo hii ndani ya miaka miwili ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Ally Mwinyi tumeshuhudia mageuzi makubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi…Juhudi hizi zimetokana na ninyi Wabunge katika kujenga hoja Bungeni,” amesema Dkt. Jafo.
Kwa upande wao Wajumbe wa kamati hiyo, wameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendesha na kutoa mafunzo ya Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ambao umeainisha wajibu na nafasi ya Wabunge na Watendaji wa Halmashauri katika kusimamia Mfuko huo.