Waratibu wa Mikoa wa Tiba Asili/Mbadala nchini wametakiwa kufanya kazi kwa lengo la kuboresha huduma za tiba asili na kusimamia vizuri masuala ya tiba asili licha ya Tanzania kuwa kubwa.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi msaidizi anayeratibu Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Paulo Mhame wakati akifungua mafunzo kwa waratibu hao jijini Dodoma.
Dkt. Mhame amesema wameona ni wakati wa kuwajenmgea uwezo waratibu hao wa Mikoa 26 kutoka Tanzania bara ili wanapokuwa kwenye majukumu yao waweze kutekeleza vizuri Sheria ya Tiba Asili Namba 23 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake na miongozo mbalimbali.
“Waratibu hawa wapo walioteuliwa hivi karibuni na wengine ni wa zamani hivyo ni fursa pia kwa wale wa zamani na hii itarahisisha utendaji kazi wakati tunapo wapatia maelekezo na hivyo kutokuwepo tena maswali mengi, hivyo hii ni fursa kwao ya kupata ufafanuzi wa maswali yao ili wabaki kutekeleza katika mikoa yao” Aliongeza Dkt. Mhame
Amesema licha ya waratibu hao kupatiwa mafunzo wataenda pia kuwa walimu kwa kuwafundisha na kuwaelekeza waratibu wa halmashauri zao na hivyo huihisha utekelezaji wa masuala ya tiba asili nchi nzima.
“Tiba asili kwa kipindi kirefu ilikua kama imelala hivyo kwa sasa tumeamua kuwa na nguvu na ari mpya na hivyo tumeanza kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi na kwa waratibu hawa tunawapatia uwezo na nyezo kwa waratibu wetu wa mikoa na halmashauri”.
Akizungumzia sheria ya Tiba Asili Namba 23 ya mwaka 2002 Dkt. Mhame amesema sheria hiyo inazungumzia zaidi tiba asili ikiwemo usajili wa watoa huduma wenyewe, wahudumu na wasaidizi wao, wauza duka na wasaidizi wao, usajili wa vituo vya kutolea huduma za tiba asili na vile vya kuuza dawa pamoja na usajili wa dawa za tiba asili baada ya kupata ridhaa au vipimo kutoka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kuhusu usajili Dkt. Mhame amesema hadi sasa wameshasajili dawa 67, vituo 1,280, waganga wa tiba asili zaidi ya 28,000 na matarajio yao ni kuweza kuwasajili wengi ili wanapokua wanazungumzia sheria wawe wanaelewa.
Naye, Msajili wa Baraza la Tiba Asili/Mbadala Dkt. Ruth Suza amesema Baraza lake linatarajia kuanza kusajili waganga wa tiba asili kwa kutumia mfumo hivyo mafunzo hayo watafundishwa pia mfumo huo na hivyo itawasaidia waratibu kuwarahisishia kuwafikia waganga wengi tofauti na zamani ambapo walikua wakijaza fomu kwenye halmashauri na kuzipeleka ngazi za chini kwa watendaji na kujadiliwa ila kwa njia hiyo watajisajili moja kwa moja.