Waziri Mkuu Mstaafu , Jaji Joseph Warioba ameamua kuingilia kati vita dhidi ya dawa za kulevya na kuwataka viongozi kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu na kufanya utafiti utakaoleta suluhisho tatizo la dawa za kulevya.
Jaji Warioba anaamini nyakati hizi si za kushughulika na waathirika wa dawa za kulevya bali kufanya tafiti ili kubaini suluhisho na kupunguza idadi ya watu kujiingiza katika dawa za kulevya, ili kuokoa taifa ambalo bado halijaathirika na dawa za kulevya.
Warioba amesema ni wakati muafaka kila mtu kusoma sheria kuhusu uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
”Jamii isidili na watu walioathirika, mnafikiri suala ni kumfunga anayetumia dawa za kulevya au anayefundishwa kutumia dawa za kulevya” amesema Warioba.
Jaji ameeleza ni vyema wananchi wakaelezwa namna ya kupambana na tatizo hilo kuliko kujikita katika siasa na watu
Amesema kuna sheria inayoeleza tatizo ni nini kuna taratibu na namna ya kuitumia basi wananchi wangefundishwa ili wafahamu kitachowasibu mara baada ya kukeuka sheria hiyo ya utumiaji dawa za kulevya.
Hivyo amesisitiza itafutwe njia ya kushughulikia tatizo la dawa za kulevya badala ya kulumbana na kutoa matamko kwani hayasaidi kumaliza tatizo