Lydia mollel – Morogoro.
Wasaidizi wa kazi za Nyumbani, wameziomba Mamlaka husika kuweka msisitizo wa mishahara yao kutokana na baadhi ya waajiri kuendelea kuwalipa ujira wao kidogo, tofauti na kiwango kilichowekwa na Serikali cha shilingi 60,000 kwa mwezi mmoja na kwamba wamekuwa wakilazimika kujigharamikia kwa baadhi ya mahitaji.
Wasaidizi hao wa Kazi, wameyasema hayo katika Semina iliyoandaliwa na shirika la The Light for Domestic Workers – LDW, Mkoani Morogoro ambayo ilikuwa ikijadili changamoto wanazokutanazo, kuwapa elimu juu ukatili, kujua haki zao na kukumbushana wajibu wawapo kazini.
Akiongea katika semina hiyo, Mkurugenzi wa LDW, Beatrice Johnson ameiomba Serikali kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa jamii, ili kumsaidia mfanyakazi wa nyumbani kulipwa mshahara stahiki na pia kutengeneza sheria zitakazo saidia kupunguza ukatili dhidi yao na jamii inayomzunguka.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Pendo Meshure amesema mbali na kuwapa elimu ya kujikinga na ukatili na kutambua haki zao za msingi, pia amewaasa kuacha tabia ya kuwafanyia ukatili watoto wanaoshi nao kwenye jamii ikiwemo kuridhika na vipato wanavyovipata, ili kuepuka kushawishika ama ukatili wa kingono.