Viongozi nchini, wametakiwa kubadili mfumo wa uchaguzi ili kuwapa nafasi vijana wa vyama vyote nchini kushiriki kukuza na kuendeleza Demokrasia badala ya kuegemea upande wa chama tawala pekee kitu ambacho kinarudisha nyumma mwangaza wa Demokrasia.
Hayo yamesemwa na Vijana na Wanawake walioshiriki katika maadhimisho ya siku ya Demokrasia Duniani, ambapo kwa Tanzania inaandika historia ya kufikisha miaka 30 ya Demokrasia ya vyama vingi tangu viliporidhiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Julai 1, 1992.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, John Pambalu amesema ushiriki wa vijana katika upande wa Demokrasia bado upo chini huku wakipewa nafasi chache za uongozi kutokana na rushwa miongoni mwa vyama vya siasa.
Amesema, “ushiriki wa vijana katika siasa kwa upande wa Tanzania sio mkubwa sana kwasababu kadhaa rushwa imetawala sana miongoni mwa vyama vya siasa tunaona iko haja ya kuongeza nguvu ya kina katika kuhakikisha kwamba vijana wanashiriki katika Demokrasia wanakuwa ni sehemu ya maamuzi ya kitaasisi ya nchi na maeneo wanayotoka”
Hata hivyo, baadhi ya vijana wamekuwa wakiamini kuwa asilimia kubwa ya vijana na wanawake wanaopatiwa nafasi za uongozi nchini wanatoka Chama cha Mapinduzi – CCM, hali inayowalazimu wengi wao kukosa chaguo sahihi na kulazimika kujiunga na chama tawala, ili waweze kufanikisha malengo waliyojiwekea.