Jamii imetakiwa kuwajenga watoto wao kiimani, ili waishi kwa hofu ya Mungu itakayowapelekea kujiepusha na vitendo viovu, ikiwemo kuchukia uhalifu na wahalifu.
Wito huo, umetolewa na afisa Polisi Jamii Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkaguzi wa Polisi, Makame Ali Makame, katika shehia ya Finya wakati alipokutana na kuzungumza na Wananchi na kuitaka jamii kuendelea kuimarisha malezi ya watoto kiimani.
Amesema, “Elimu ya kiroho inamjenga mtu kuwa mnyenyekevu, mpenda haki na muadilifu hivyo itawaepusha watoto wenu kutofanya matendo maovu kwa kuelewa kufanya hivyo ni kosa kwa wanadamu na mbele ya Mungu.”
Kwa upande wake afisa Polisi jamii Wilaya ya Wete, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Masoud Ramadhan aliwataka wananchi hao kushiriki katika vikundi vya ulinzi shirikishi katika mitaa yao ili kuweza kudhibiti uhalifu kwa ngazi ya awali kwani wao ndio wanaishi katika jamii hiyo na wanafahamiana.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Amina Haji Sipe aliwataka wananchi hao kutovifumbia macho vitendo viovu katika jamii ikiwa ni pamoja na vitendo vya udhalilishaji ili wahalifu wapatikane na kisha wafikishwe katika vyombo vya sheria.