Mabingwa wa Shelisheli, Timu ya Saint Louis, tayari wapo nchini na wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Jijini Dar es salaam, kwaajili ya kuwakabili mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika itakayopigwa Jumamosi.
Saint Louis inayonolewa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shelisheli, Ulric Mathiot kufuatia kujiuzulu kwa kocha mkuu aliyekosa leseni A ya CAF, inaonekana imefanya utafiti kuhusu Yanga na soka la Tanzania kwa ujumla ambapo Mathiot amekiri kuwa kiwango cha soka la Tanzania kiko juu kuliko Shelisheli na kusema kuwa lolote linaweza kutokea.
“Nimeona video chache za mechi zao, lakini unajua, kama natakiwa kulinganisha kiwango ni ngumu sana kwasababu Shelisheli tupo kiwango cha chini. Nimewahi kuja hapa, nimewaona Azam wakicheza, nimewaona Simba, najua hapa ni soka la juu sana, lakini katika mechi ya mpira wa miguu, huwezi jua, kama umejiandaa vizuri kwa kiwango chako, lolote linaweza kutokea,” amesema mkurugenzi huyo.
Naye nahodha wa Saint Louis Bertrand Esther amekiri ugumu kwenye mtanange huo, lakini amesema watajituma kutafuta matokeo mazuri kabla ya kurudiana wiki moja baadaye nchini Shelisheli.
Kwa upande wao Yanga wanaendelea na maandalizi ya mchezo huo huku wakikabiliwa na majeruhi wengi wa kikosi cha kwanza, lakini bado wachezaji waliopo wanaonekana kuwa na muunganiko mzuri.