Watu saba akiwamo mwanamke mmoja wanashikiliwa na Polisi jijini Arusha kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii.
Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo, ambapo amesema kuwa watu hao wamekamatwa kutokana na sababu za kuhamasisha maandamano Aprili 26 mwaka huu.
Amesema kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakihamasishana kwa kutumia mitandao ya kijamii ikiwamo ya Telegram na WhatsApp.
Amesema watu hao wamekamatwa kupitia vitengo vya intelijensia baada ya kuwekewa mitego mbalimbali na kufanikiwa kuwakamata.
Aidha, amesema miongoni mwa watuhumiwa hao baadhi yao ni wanafunzi wa vyuo vikuu, mitaani na maeneo mengine.
“Nasisitiza hakuna maandamano Aprili 26, atakayeandamana atavuna alichopanda kwa kuwa Serikali haijaribiwi,” amesema Kamanda Ilembo
Hata hivyo, Ilembo ameongeza kuwa watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote, huku wakiendelea kuwatafuta wengine kwa njia mbalimbali.