Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kiasi cha Shilingi bilioni 35.07 kimepatikana baada ya washtakiwa mbalimbali kukiri makosa.
Profesa Kabudi ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Aprili 28, 2021 wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Amesema Wizara kupitia ofisi ya Taifa ya mashtaka imeendelea kutekeleza zoezi la makubaliano ya kumaliza kesi za jinai chini ya utaratibu wa washtakiwa kukiri makosa yao kwa mujibu wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba 11 ya mwaka 2019.
Amesema katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021, kesi 192 zilihitimishwa kwa njia hiyo.
Aidha, Profesa Kabudi amesema jumla ya washtakiwa 243 walikiri makosa na kulipa serikalini kiasi Sh. bilioni 35.07 kama fidia pamoja na faini kutokana na makosa ya uhujumu uchumi.
“Zoezi hili ni endelevu na fedha hizi zimewekwa katika akaunti maalum iliyoko Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Prof. Kabudi.