Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam imewafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa watano waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kujiunganishia bomba la mafuta mali ya Mamlaka ya Bandari (TPA) isivyo halali.
Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 23, 2019 na Hakimu Mkazi mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania DPP kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Audai Ismail, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.
Inadaiwa mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, washtakiwa hao walijiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali.