Kesi ya kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji “MO” imesikilizwa tena hii leo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, huku upande wa utetezi ukiomba jitihada za kusakwa kwa washtakiwa wengine watano ili kuunganishwa na mshtakiwa Mousa Twaleb.
“MO” alitekwa nyara Oktoba 11 mwaka 2018 alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana, Dar es salaam.
Wakili wa Utetezi, Robert Mtakula ameuomba upande wa mashtaka kuongeza jitihada za kuwatafuta washtakiwa watano waliomteka mfanyabiashara huyo ambaye pia ni muwekezaji wa klabu ya klabu ya soka ya Simba.
Mshitakiwa Twaleb ambaye ni dereva taxi ni mkazi wa Tegeta tayari alishafikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa utetezi Mtakula alidai kuwa hati ya kukamatwa kwa washtakiwa hao ilishatolewa na mahakama ninaomba jitihada zifanywe ili kuhakikisha wanakamatwa ili shauri hilo liweze kuendelea.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simoni kudai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao, hivyo wanaendelea kuwatafuta na wataieleza mahakama hatua waliyofikia.
Awali mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini.
Hata hivyo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30, 2019.