Wasichana wawili ambao wana uhusiano wa kimapenzi kwa wakati mmoja na Mfalme wa RnB, R Kelly na ambao wako katika orodha ya wanaodaiwa kudhalilishwa kingono wamejitokeza kumtetea dhidi ya tuhuma hizo.

Joycelyn Savage  na Azriel Clary wamejitokeza kwa pamoja ikiwa ni siku moja tangu R Kelly afanye mahojiano yaliyomtoa machozi akipinga kufanya vitendo hivyo huku akikabiliwa na kesi ya kuwadhalilisha wanawake kadhaa, wanne kati yao wakidaiwa kuwa walikuwa chini ya umri wa miaka 18 wakati alipowafanyia vitendo hivyo.

Warembo hao wamedai kuwa wote wanampenda R Kelly na wanafahamu kuwa ana uhusiano nao kwa wakati mmoja na hawajali hilo kwani kuna watu wengi duniani wana wapenzi zaidi ya mmoja.

“Sisi tuko kwenye mapenzi na R Kelly na wote tunampenda, tunajua ni kawaida kwa sababu kuna watu wengi tu huko duniani wana wapenzi zaidi ya mmoja,” alisema Clary huku Joycelyn akitikisa kichwa kuonesha kukubali.

Azriel Clary ambaye baba yake alifanya mahojiano na vyombo vya habari akieleza kuwa R Kelly amemchanganya akili mwanaye huyo na kunyanyasa kingono, amekana madai ya baba yake akimuita muongo na tapeli.

Amesema baba yake alishirikiana na mama yake kumtumia kutaka kumtega R Kelly wakimtaka ajitahidi kupiga naye picha zenye muonekano wa kingono ili wazitumie baadaye kumtishia na kumdai pesa.

“Sikumuangalia usoni baba kwa sababu ni muongo na tapeli. Huo ni uongo mkubwa, sikuwahi kufanya mapenzi na R Kelly nikiwa na umri wa miaka 17,” alisema Clary.

“Nilipokutana na R Kelly, mama yangu na baba walitaka nimdanganye kuhusu umri wangu, na alidhani kuwa nina miaka 18 lakini nilikuwa na miaka 17. Na zaidi ya hapo, wazazi wangu walikuwa wanataka nichukue picha za ngono na R Kelly ili wazitumie baadaye kumtishia wakimuomba pesa,” aliongeza Clary.

Madai kama hayo pia yalitolewa na Joycelyn Savage ambaye amewashutumu wazazi wake kuongopa ili wajipatie pesa kupitia sakata la R Kelly.

Wote kwa pamoja walikosoa vikali maelezo ya wazazi wao waliozungumza kwenye makala ya ‘Surviving R Kelly’ wakidai kuwa mwimbaji huyo aliwageuza watoto wao kuwa wafungwa wa ngono.

Hata hivyo, wakati R Kelly anajitetea na kutetewa, jana alikumbwa na pigo lingine baada ya kukamatwa kwa kosa la kutotoa matunzo ya watoto wake ya kiasi cha $161,000 na anaendelea kushikiliwa polisi.

Mwimbaji huyo yuko kwenye wakati mgumu katika kipindi ambacho makala maalum ya ‘Surviving R Kelly’ imeibua maovu mengi anayodaiwa kuyafanya ndani ya kipindi cha miongo miwili.

Hospitali ya Kibena yakabiliwa na changamoto ya watoto Njiti
Neville: Solskjaer atachagua mshahara, ataweka sanamu yake

Comments

comments