Watu wasiojulikana, wakiwa na Silaha wamewaua takriban watu 23, na kuwajeruhi wengine 12 katika shambulio lililofanywa katika kijiji kimoja katikati mwa nchi ya Mali.
Gavana wa jimbo la Bandiagara ambako shambulio hilo lilifanyika, Sidi Mohamed El Bechir amesema watu hao wasiojulikana walifanya mauaji hayo na kisha kuchoma moto nyumba kadhaa katika kijiji cha Yarou.
Awali, Rais wa Shirika la Vijana wa eneo hilo, Amadou Lougue alisema, “washambuliaji hawa walikaa kijijini hapo hadi saa 7 mchana, na kuteketeza sehemu ya kijiji, kuvunja maduka na kuchukua Ng’ombe wa wanakijiji.”
Jamii za eneo la kati na kaskazini mwa Mali zimekuwa katika mzozo wa ghasia za muda mrefu za kutumia silaha tangu mwaka 2012, huku Waasi wenye itikadi kali wakilazimishwa kuondoka madarakani katika miji ya kaskazini mwa taifa hilo la Afrika Magharibi mwaka uliofuata kwa msaada wa operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Ufaransa.