Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, imepitisha rasimu ya sheria ndogo inayotaka Wazazi watakaoshindwa kuwalipia vyakula watoto wao wakiwa shuleni, wafungwe miaka miwili gerezani.
Hayo yamesemwa na na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Sifael Kulanga ambapo ameeleza kuwa rasimu hiyo inaandaliwa mchakato kupitishwa na rasmi na Waziri mwenye dhamana ili iwe sheria kamili.
Katika rasimu hiyo, inaonesha mzazi anaweza kutozwa faini isiyopungua shilingi 200,000 na isiyozidi milioni moja au kifungo kisichopungua miezi 12 na kisichozidi miezi 24 au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Kulanga amesema, rasimu hiyo imelenga kuhakikisha wanafunzi kuanzia awali hadi sekondari wanapata chakula Shule kama moja ya jitihada za kuongeza viwango vya taaluma shuleni.
“Katika rasimu hii, wazazi watalipa kiasi cha Sh 70,000 kwa mwaka ikiwa ni Sh 35,000 kwa muhula kwa wanafunzi wa awali, Sh 90,000 kwa mwaka kwa elimu ya msingi na Sh 120,000 kwa sekondari kwa mwaka” amesema
Aidha, ameeleza kuwa fedha za chakula shuleni zitasimiwa na wazazi wenyewe kupitia kamati watakazounda lakini kamati hizo zinaweza kuvunjwa na mkurugenzi wa Manispaa iwapo zitaenda kinyume na malengo.
Meya wa Manispaa hiyo, Mhandisi Zuberi Kidumo alisema baada ya waziri kutangaza sheria hiyo katika gazeti la serikali itaanza kutumika rasmi na itakuwa lazima wazazi kutoa michango hiyo.