Polisi wa Sharia ya Kiislamu katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la ”The Islamic Sharia Kano’ wamewakamata kwa muda watu 80 waliotuhumiwa kwa kula hadharani, badala ya kufunga kuanzia alfajiri hadi jua linapotua kulingana na maagizo ya dini ya kiislamu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Polisi wa Sharia , wanaofahamika kama Hisbah, wamesema kuwa watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbali mbali ya mji wa Kano katika kipindi cha siku kadhaa.
Aidha, Jimbo la Kano ni moja kati ya majimbo kadhaa ya kaskazini mwa Nigeria ambako Sharia ya Kiislamu iliyoanzishwa upya tangu mwaka 2000, ambapo Sharia ya Kiislamu inatekelezwa sambamba na sheria ya kawaida kwenye majimbo hayo.
Msemaji wa Hisbah katika jimbo la Kano, Adamu Yahaya amesema kuwa wote waliokamatwa walikuwa ni Waislamu na maafisa hawawalengi wasio Waislamu kwasababu hawafungwi na sheria ya Kiislamu.
Amesema kuwa baadhi ya wale waliokamatwa waliiambia ofisi ya Sharia kuwa walikuwa wanakula kwasababu hawakuuona binafsi mwezi wa Ramadhani huku wengine wakisema walikuwa ni wagonjwa, lakini maafisa walisema kuwa madai yao hayakuwa na msingi wowote.
Hata hivyo, watu hao 80 walionywa na kuachiliwa huru kwasababu walikuwa wamefanya kosa hilo kwa mara ya kwanza.
Mfungo wa Ramadani ni lazima kwa kila mtu mzima Muislamu lakini baadhi ya watu kama vile wenye magonjwa makubwa hawatakiwi kufunga.