Wataalam wa afya 60 kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo ya kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilimia 50.


Elimu hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mafunzo maalum ya siku mbili ya jinsi ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa yaliyoandaliwa na kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura na kufanyika katika ukumbi wa JKCI leo Jijini Dar es Salaam.

Prof. Janabi


Akizungumza katika mafunzo hayo Prof. Janabi ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo amesema kuwa JKCI iliona ni muhimu kwa wataalamu hao wa afya kupata elimu ya kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilima 50 kwani wengi wao wametoka katika hospitali za wilaya ambazo wagonjwa huanzia huko.


“Tumetoa elimu ya kutambua moyo unaofanya kazi chini ya asilimia 50 kwa wataalam wa afya wanaoshiriki mafunzo ya jinsi ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa kwani hawa ndio wataalam wanaokutana na wagonjwa wengi katika ngazi ya kwanza hivyo kupitia elimu niliyoitoa itawasaidia zaidi kutoa huduma bora za matibabu wanapokutana na wagonjwa wa moyo lakini pia kutambua ni kwa wakati gani wanapaswa kuwapa rufaa wagonjwa hao kufika katika taasisi yetu,” alisema Prof. Janabi.


Akizungumzia mafunzo ya dharura kwa wagonjwa Prof Janabi amesema kuwa wataalam wa afya wanaopata mafunzo hayo itawasaidia kutoa huduma ya dharura iliyo sahihi kwani hatua ya kwanza kufanyiwa mtu anayehitaji huduma ya dharura ni ya muhimu kama itafanywa kwa usahihi hivyo kuokoa maisha ya mgonjwa.

Wataalamu wakiwa mafunzoni.


“Kupata ujuzi wa jinsi ya kutoa huduma ya kwanza haimtaki mtu kuwa daktari tu bali kila mtu anapaswa kuwa na ufahamu wa kutoa huduma hiyo kwani kwa kuwa na ujuzi huo humsaidia mtu kuokoa maisha ya mtu mwingine anayehitaji huduma ya dharura mahali popote pale tatizo linapojitokeza,”


“Iliwahi kunikuta mara mbili nikiwa katika safari tofauti nimeweza kuokoa maisha wa watu wawili waliohitaji huduma ya dharura hivyo kuokoa maisha yao, ndio maana nasisitiza watu wote tuwe na ufahamu wa namna ya kutoa huduma ya dharura kwani dharura hizo hazitokei hospitali peke yake,” alisema Prof. Janabi.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanahusisha wataalamu kutoka hospitali za wilaya na za binafsi za jiji la Dar es Salaam.

Maambukizi ya Ukoma yashuka chini ya 5% Tanzania
Daraja la Tanzanite kuanza kutumika Februari 1